KARIBU

Thursday, February 2, 2012

wabunge waigomea serikali

WABUNGE wamekataa kupitisha azimio la Serikali la kupunguza ushuru wa maji ya chupa kutoka sh. 69/- hadi Sh. 12/- kwa chupa kwa kuwa punguzo hilo halitamnufaisha mwananchi wa kawaida.

Wabunge wametoa msimamo huo leo mchana baada ya Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, kumaliza kujibu hoja za wabunge waliochangia hoja ya Azimio la Bunge la Kuridhia Marekebisho ya Jedwali la Nne la Sheria ya Ushuru wa Bidhaa sura ya 147 iliyowasilishwa bungeni leo asubuhi.

Baada ya Mkulo kumaliza kujibu hoja hizo na kuwaomba wabunge wapitishe azimio hilo, Mbunge wa Buchosa, Dk. Charles Tizeba (CCM), aliomba mwongozo na kutaka hoja hiyo iondolewe kwa kuwa haina manufaa kwa mlaji wa mwisho.

Dk. Tizeba amesema, punguzo hilo halitamnufaisha mwananchi kwa kuwa halitekelezeki kwenye soko la rejareja hivyo iondolewe, ijumuishwe kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha.

Amesema, punguzo hilo litawanufaisha wenye viwanda na akamkariri Waziri Mkulo kuwa amewasilisha hoja hiyo baada ya kushawishiwa.

Baada ya Mbunge huyo kutoa hoja yake, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema, Dk. Tizeba hakutumia kanuni sahihi kuwasilisha hoja yake lakini kanuni za Bunge zinatoa fursa kwake kuwahoji wabunge kama wanaunga mkono hoja ya msingi au la.

Aliwahoji wabunge, wengi wakaikataa hoja ya Serikali. “Wasioafiki wameshinda, kwa hiyo itabidi tujipange upya wakati mwingine kadri hali itakavyoruhusu” amesema Ndugai.

Kabla ya wabunge kugoma kupitisha azimo hilo, wabunge walitoa mawazo tofauti kuhusu punguzo hilo wakiwemo waliounga mkono na kuna waliopinga.

Mbunge wa Viti Maalum, Leticia Nyerere (Chadema), aliipongeza Serikali kwa kuwa sikivu na kuwasilisha azimio la punguzo hilo la ushuru wa maji ya chupa litakaloikosesha serikali mapato ya takribani shilingi bilioni 7.7/-

Amesema , umefika wakati kwa Serikali kuwa sikivu na ichukue mawazo bila kujali anayetoa anatoka chama gani. “Tunaruhusu tofauti ambazo hazileti mantiki katika maendeleo ya Taifa letu” amesema Mbunge huyo.

Dk. Tizeba ameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuvilinda viwanda vya ndani lakini akamtaka Waziri Mkulo alieleze Bunge kwa nini alikaidi ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi kuhusu suala hilo.

Mbunge amesema bungeni kuwa, wajumbe wa kamati hiyo ni Watanzania na wana mapenzi na nchi yao hivyo Mkulo aseme limepata hasara kiasi gani kwa kukaidi ushauri wa kamati hiyo.
“Niseme tu kwamba huu ni mwenendo mzuri” amesema Dk. Tizeba na akaongeza kwamba, hana uhakika kama kuwasilisha azimio hilo sasa ni usikivu .

Mkulo ameomba radhi kwa niaba ya Serikali kwa kuchelewa kuwasilisha azimio hilo, na kwamba, haikuwa dhamira ya Serikali au uzembe ila hali halisi. Amesema, punguzo hilo la ushuru halitakuwa na athari yoyote kwa uchumi wa nchi na litawasaidia wananchi kwa kiasi fulani.

Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM) amesema, ni aibu kuagiza maji kutoka nje ya nchi, na amedai kuwa hakuna dhamira ya kutosha kulinda viwanda vya ndani.

Amependekeza kuongezwa kwa ushuru kwa maji yanayoagizwa kutoka nje ya nchi na akadai kuwa mwenendo wa kuagiza bidhaa kutoka nje ukiendelea fedha ya Tanzania haitakuwa imara.

“Leo hii tunapozungumzia maji tunazungumzia uchumi wa nchi” amesema Mbunge huyo na kupinga kupunguza matumizi mengine ya Serikali.

Mkulo amesema, maji ya chupa yanayotoka nje ni asilimia 20 ya maji yanayotumiwa nchini na kwamba, kupunguza matumizi ya Serikali si jambo jipya kwa kuwa lilishazungumzwa hata kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha 2011/ 2012.

Mbunge wa Viti Maalum, Zarina Madabida (CCM) ameipongeza Serikali kwa kulinda viwanda vya ndani lakini amehoji punguzo hilo linamsaidia nani.

Madabida amesema, punguzo hilo ni dogo sana kwa mlaji wa mwisho, hivyo amependekeza ushuru wa bidhaa kutoka nje uongezwe na ikiwezekana zizuiwe kuingizwa nchini.

Amesema, kupunguza ushuru kutoka sh. 69/- hadi sh. 12/- kwa chupa ya maji ni sawa na kupunguza sh. 57 tu kwa mlaji wa mwisho hivyo hakutamletea nafuu yoyote hivyo amekataa kuunga mkono hoja hiyo.

Mbunge wa Kalenga, William Mgimwa (CCM), amesema, kitendo cha serikali kuendelea kutoza ushuru wa sh. 69/- kwa chupa ya maji inayozalishwa nchini ilikuwa ni kukaidi ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi.

Amemtaka Waziri wa Fedha atafute namna ya kufidia punguzo hilo na aseme athari za uamuzi huo.

Mbunge wa Lushoto, Henry Shekifu (CCM), ameitaka Wizara ya Fedha itafute vyanzo vingine vya mapato na iongeze ushuru kwa maji yanayotoka nje ya nchi.

Amemtaka Waziri wa Fedha atafute vyanzo vingine vya mapato badala ya kukata matumizi serikalini kwa kuwa kutaifanya Serikali ishindwe kujiendesha na kushinda pia kuwadhibiti watendaji.

 
     

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Facebook Themes