KARIBU

Thursday, February 2, 2012

okwi ainogesha simba

ImageSIMBA jana ilizidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya kuifunga JKT Oljoro mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Hata hivyo iliichukua Simba mpaka dakika ya 60 kupata bao hilo lililofungwa na Emmanuel Okwi aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya Davies Kago. Okwi alifunga bao hilo kwa kumalizia
kazi ya Uhuru Selemani aliyekuwa akiwatoka mabeki wa Oljoro toka upande wa kushoto.

Okwi aliwainua tena mashabiki wa Simba vitini katika dakika ya 83 baada ya kufunga bao la pili kwa kazi nzuri ya Uhuru aliyemtengea mpira kabla ya kuujaza wavuni. Matokeo hayo yanaifanya Simba kuendelea kutesa kileleni ikiwa na pointi 34 huku mpinzani wake wa jadi Yanga ikiwa na pointi 31.

Simba ilicheza mechi hiyo pungufu karibu muda wote wa kipindi cha pili baada ya
mwamuzi Isihaka Shirikisho kumpa Haruna Moshi 'Boban' kadi nyekundu kwa kumchezea
rafu Omari Mtaki katika dakika ya 43.

Baada ya kadi hiyo wachezaji wa Simba walimzonga mwamuzi hali iliyolazimu mchezo kusimama kwa muda, kwa ujumla katika mechi hiyo, hasa kipindi cha kwanza wachezaji wa pande zote mbili walichezeana kibabe.

Kabla ya kadi hiyo, Boban, Mwinyi Kazimoto na chipukizi Jonas Gerald walishirikiana vema katikati na kutengeneza nafasi kadhaa ambazo zilizuiwa na ngome ya Oljoro chini ya Mtaki.

Dakika ya 71 nusura kipa wa Simba Juma Kaseja aiponze timu yake kutokana na mbwembwe zake alipokuwa akiuchezea mpira ukawahiwa na washambuliaji wa Oljoro shukrani kwa beki Kelvin Yondani aliyewahi kuukoa mpira huo uliokuwa ukielekea wavuni.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Facebook Themes